The following is the handout prepared by Sarah Kanza (project intern in Mwanga) for farmers for the training sessions delivered at the beginning of the new cycle of vegetable growing in June 2025.
MAGONJWA NA WADUDU, NA UDHIBITI WAKE
Kupambana na wadudu na magonjwa kwa njia asilia
Kuna aina mbalimbali za magonjwa, virus, bacteria, ukungu, kutu na wadudu wanaoshambulia mazao shambani. Ni muhimu kuzitambua ili kuweza kukabiliana.
Magonjwa ya virusi
… kama vile batobato hushambulia majani, na husababisha majani ya kijani kuwa na rangi ya njano na kukunjamana. Virusi vya streak (michirizi ya njano kwenye mahindi) husababisha mmea kutokukua vizuri na kutoa mazao hafifu. Virusi vya leaf curl husababisha majani kuwa ya njano na kujikunja kuelekea chini. Hakuna dawa ya kutibu magonjwa ya virusi katika mimea. Njia bora ni:
- Kuzungusha mazao shambani
- Ng’oa na choma mimea iliyoathirika
- Tumia mbegu bora ambazo hazijaathirika na ugonjwa
- Tumia matandazo kama vile nyasi kavu huzuia magugu kuota kwa kasi .
- Kudhibiti wadudu wanaoeneza virusi


Baadhi ya magonjwa ya bakteria
… yanayoshambulia mimea ni:
- Mnyauko (wilting)
- Madoa madoa kwenye majani (leaf spots)
- Kuoza kwa matunda (fruit rot)
- Baka jani (leaf blight)
- Canker ya bakteria (bacterial canker)
Ingawa dawa nyingi za asili haziwezi kuua bakteria moja kwa moja, zinaweza kusaidia kuzuia maambukizi mapya (mfano: mwarobaini, pilipili, vitunguu saumu.


MAGONJWA ya fungus (ukungu) na kutu
Hushambulia mazao yote — matunda, mboga za majani, na sehemu mbalimbali za mmea kama shina, majani, na matunda. Moja ya dalili za ukungu ni mashambulizi kwenye shina, majani au matunda, na mara nyingi husababisha mmea kunyauka au kuoza.


Namna ya kuzuia ukungu na kutu Kwa magonjwa ya fungus kama ukungu mweupe (powdery mildew) au ukungu laini (downy mildew) tunaweza kutumia njia zifuatazo:
- Maziwa fresh: Changanya lita 1 ya maziwa fresh na lita 12 za maji, kisha ongeza kijiko kimoja cha sabuni ya unga. Koroga vizuri kisha nyunyiza kwenye mmea kila baada ya wiki moja.
- Mchanganyiko wa kitunguu swaumu na pilipili. Changanya vitunguu swaumu punje 10, pilipili kali 5 kulingana na ukubwa uliopata, maji lita 1, saga mchanganyiko hadi upate uji mzito kisha chuja vizuri, tumia kila baada ya siku 7-15. Hii husaidia kuua wadudu (aphids) na konokono.
- Tumia mkojo wa ng’ombe weka mkojo wa ng’ombe siku 14, chukua lita moja ya mkojo wa ngombe changanya na maji lita 6, ongeza kijiko kimoja cha sabuni ya unga changanya vizuri kisha nyunyiza kwemye mmea kwa wiki mara moja.
- Baking soda (bi-carbonate soda): 100gm, weka maji lita 10, nyunyuzia kwenye mmea wakati wa jioni.
- Majani ya papai mabichi yanaweza kutumika, kwa kusaga majani kiasi cha 1kg changanya na maji kiasi cha lita 1,tikisa vizuri kisha chuja mchanganyiko huu,kisha ongeza maji lita 4,vijiko 2 vya kerosine na sabuni kiasi cha kijiko kidogo kisha puliza kuua funza wakataji wa mazao.
Wadudu kama vile viwavi jeshi vamizi, viwavi kikataji
Wadudu hawa hushambualia majani ya mmea hivyo ni muhimu kuwahi kupiga dawa kabla ya uvamizi wa wadudu,mara nyingi wadudu hushambualia mazao wakati wa usiku na alfajiri hivyo tunashauriwa kupiga dawa mara kwa mara wakati wa jioni au asubuhi.
Namna ya kuzuia wadudu wasumbufu wa mazao
Changanya mazao: hasa mazao yenye kufukuza wadudu kama vile repellant plants mfano marigold, pilipili, kitunguu swaumu au kitunguu maji.
Tumia dawa za asili:
Mwarobaini: Tumia mbegu na majani ya mwarobaini saga 1kg ,kisha loweka kwenye maji kupata lita 1 ya mchanganyiko. Changanya na maji lita 12. Ongeza kiijko kimoja cha sabuni ya unga. Tumia mchanganyiko huu kunyunyiza kwenye mmea kila baada ya siku 7. Hii husaidia kufukuza wadudu kwa kiasi kikubwa. Tunashauriwa kuepuka matumizi ya mazao au mboga punde tu baada ya kunyunyiza dawa hivyo basi ni vizuri kutumia mazao haya baada ya siku 7 tokea kunyunyiza dawa
Dawa ya pilipili: Kata 1kg ya pilipili kali kisha chemsha.Chukua 1/2kg ya mchemsho changanya na maji lita 15-20. Ongeza kijiko kimoja cha sabuni ya unga.Nyunyiza kila baada ya siku 7.Unga wa pilipili kali pia unaweza kutumika.nyunyiza kuzungaka shina la mmea kuzuia mchwa,minyoo wakataji,konokono.Mchanganyiko huu huzuia virusi vya batobato(mosaic) na kuzuia kusambaa kwa virusi wengine,pia pilipili hutumika kugukuza wadudu waharibifu wa mazao.
Mkojo wa sungura: Chukua mkojo wa sungura kisha hifadhi kwa muda wa wiki mbili,changanya mkojo wa sungura lita 2 kwa maji lita 10,kisha nyunyuzia kwenye mmea, pia hutumika kama booster kukuzia mazao.
Mkojo wa ng’ombe na majivu: Changanya mkojo wa ng’ombe na majivu mkono mmoja,nyunyiza mchanganyiko huu kwenye mazao kila baada ya siku 7. Majivu husaidia kudhibiti wadudu wenye ngozi laini kama Aphids na pia huzuia konokono na slugs.Pia yanaweza kusaidia magonjwa ya ukungu kama mildew.Majivu ya kuni yana kiasi tofauti cha potashi(caustic potash) ambayo inaweza kuathiri mimea. Usitumie dawa hii wakati wa jua kali,na epuka majivu kugusa moja kwa moja shina la mmea hasa miche.
Kimiminika Cha alovera, pilipili kichaa (mbichi): Tumia majani 3 ya alovera ,changanya na pilipili kichaa 5-10,sabuni ya mche kiasi cha kijiko kidogo changanya na maji lita 1 kisha chuja mchanganyiko huu vizuri,nyunyiza kwenye mmea kila baada ya siku 7. Lenga maeneo yanayoshambuliwa na wadudu hasa chini ya majani
Kitunguu saumu: Dawa halisi kwa panya, menya na pondaponda punje 3 za kitunguu swaumu weka kwenye glass (sio bati) changanya kimiminika cha parafin kiasi cha kutosha kufunika vitunguu swaumu,kisha loweka mchanganyiko huu kwa siku mbili,baada ya siku mbili chuja mchanganyiko changanya na mji ya sabuni lita 10 kisha puliza kwenye mmea,weka dawa hii mbali na watoto pia epuka kutumia wakati wa mcha na kwenye miche changa.
Mtembo (Lantana Camara): Tumia majini mabichi ya mtembo kiasi cha kg 1,kisha osha majani ya lantana ili kuondoa vumbi au uchafu,saga majani haya kwenye kinu hadi yapate kua uji mzito,kisha changanya uji huo na kiasi cha maji lita 5, loweka kwa muda wa saa 12 -24 kisha chuja mchanganyiko huu,ongeza sabunui ya mche kidogo husaidia dawa kushika kwenye majani,kisha puliza kwenye mazao kila baada ya siku 7. Dawa hii hufukuza na kuua wadudu kama viwavi,Aphids na whiteflies.
Maelekezo ya kutumia dawa asilia shambani: Wakati wa kunyunyiza dawa, hakikisha majani yote ya mmea, hasa sehemu ya chini ya majani, yamefikiwa na dawa kwani wadudu wengi hujificha chini ya majani ili kujikinga na jua.
- Tunashauriwa kupiga au kunyunyiza dawa wakati wa jioni, kwani huo ndio wakati wadudu wengi hushambulia mazao.
- Tunashauriwa kutumia vifaa kama glovu ili kuzuia muwasho wakati wa maandalizi ya dawa
- Tumia barakoa au leso hasa wakati unatumia viungo vyenye ukali kama pilipili na alovera
Sources: SAT Basic organic agriculture course; Fruits and nuts, Species with potential for Tanzania (A. Nyambo et al).
